Spika wa Bunge, Anne Makinda, amesema shughuli za Bunge ni mzigo mzito.
Hata hivyo, amesema uwajibikaji wa watumishi wa muhimili huo wamemwezesha kufanya kazi zake vizuri.
Makinda aliyasema hayo juzi usiku wakati wa hafla ya kuwaaga wafanyakazi waliostaafu na kuwakaribisha waajiriwa wapya wa Bunge.
Makinda hakueleza kwa undani namna
shughuli za Bunge zinavyokuwa mzigo, lakini mara kadhaa, uongozi wake
umekuwa ukikosolewa ndani na nje ya chombo hicho cha uwakilishi wa
wananchi.
Aidha, aliwataka watumishi wapya,
kuwaheshimu wabunge na kujitahidi kutowakosea wakati wa utendaji wao wa
kazi ili kuepuka malalamiko.
“Hata kama wamefanya vibaya wao, omba samahani maana ukimjibu vibaya itakuwa nongwa tena nongwa kweli kweli,”alisema.
Makinda aliwataka watumishi wa Bunge
waliostaafu, kujishughulisha na miradi mbalimbali ya maendeleo
itakayosaidia kuwaongezea kipato badala ya kukaa bila kazi.
“Mzee wa miaka 60 si mzee anayeweza
kufanya kazi nyingine kama kuuza mitumba, nyanya…msifunge akili zenu kwa
sababu kuishi na wenzenu waliowazunguka vizuri kutafanya
msizeeke,”alisema.
Makinda aliwasihi wastaafu hao kuweka fedha zao za mafao benki ili wapate muda wa kufikiria watazitumia vipi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa
Utawala wa Bunge, Kitolipa Kipa, alisema jumla ya watumishi 19
wameajiriwa na 13 wamestaafu.
“Wenzetu tunaowaaga leo (juzi) walifanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na baada ya kupita katika misukosuko, na dhoruba,”alisema.
Aidha, aliwataka wafanyakazi wapya kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili waweze kulijenga Taifa.
Katika hafla hiyo pamoja na zawadi nyingine kila mtumishi alizawadia shilingi milioni 8.1.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
0 comments:
Post a Comment