|
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Elias Lali |
SILAHA, zaidi ya 80 za kivita zikiwemo aina ya SMG na AK 47 zimesalimishwa kwa polisi na wananchi wa vijiji mbalimbali katika
tarafa ya Sale na Loliondo Wilayani
Ngorongoro Mkoani Arusha.
Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Elias Wawa Lali
alisema kuwa silaha hizo zimesalimishwa polisi kufuatia kampeni ya kuwataka watu
wanaomiliki silaha kinyume na sheria kuzisalimisha kabla ya kukamatwa na
kufikishwa mahakamani.
Alieleza kuwa silaha hizo zimekuwa zikitumika katika
ugomvi kati ya wamasai na wasonjo hali ambayo ilikuwa inatishia hali ya usalama
katika eneo la Loliondo.
“Watu wengi wakiwemo wanawake na watoto wamekuwa wahanga
wakubwa wa migogoro hii ,serikali sasa imeazimia kumaliza migogoro hii kwa
kutumia njia zote zikiwemo za usuluhishi na kisheria”alisema.
Alisema kuwa katika operesheni hiyo watu saba
wanashikiliwa na polisi kwa thuma za kukutwa na ngombe ishirini na tisa mali ya
wafugaji wa kimasai ambao waliporwa mwezi September mwaka huu katika kijiji cha
Naan.
“ Majina yao tutayatoa baadaye ila ngombe
walioporwa katika tukio hilo tumezikamata ndani ya msitu katika eneo la
wasonjo na tayari wamiliki wake wamezitambua na watuhumiwa tayari wapo mikononi mwa
polisi”alisema Lali.
Lali aliongeza kuwa serikali Wilayani humo
inaendelea kutoa elimu na ushawishi kupitia taasisi zake ili kuwafanya wananchi
kuelewa kuwa kumiliki silaha bila kibali cha kisheria ni kosa la jinai.
“Tunafanya kila tunaloweza kutokomeza tabia ya watu kujimilikisha silaha ,nchi yetu
inaongozwa kwa utawala wa sheria haiwezekani wananchi wa kawaida kumiliki
silaha za kivita”alisema Lali.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya aliongeza kuwa
serikali inatarajiwa kutuma msuluhishi wa migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ndio
chanzo cha vita vya Wamasai na Wasonjo vita ambavyo vimegharimu maisha ya watu
wengi.
“Wakati wowote wizara itamleta msuluhishi wa migogoro
ya mipaka katika eneo lote la Lolindo ,tunaamini suala la mipaka likipatiwa
ufumbuzi migogoro na vita vitakwisha katika eneo hili”alisema Lali.
0 comments:
Post a Comment