WAFUGAJI Mkoani Arusha wametaka
serikali na wadau wa maendeleo kuelimisha viongozi wa serikali za vijiji juu
ya sheria ya ardhi na matumizi bora ya ardhi.
Wanadai kuwa ufahamu wa sheria hasa
ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999
itasaidia kuondoa migogoro ya
ardhi kati ya wafugaji ,wakulima na wawekezaji.
Wafugaji hao walisema ufahamu mdogo wa viongozi wa serikali za vijiji juu ya sheria ya ardhi umesababisha kushindwa kutengeneza matumizi
bora ya ardhi na kusababisha kuwepo kwa mgogoro mingi katika jamii.
Mwenyekiti
wa kijiji cha Losirwa Wilayani Monduli George Lukas alisema kuwa vijiji vingi
havijatenga maeneo kulingana na makundi mbalimbali zikiwemo sehemu za malisho
na za kilimo.
“Ni lazima viongozi wa serikali za vijiji
waelimishwe kutenga maeneo kulingana na na mahitaji yaliyopo na kuhakikisha
kuwa wanasimamia sheria ya ardhi”alisema Lukas.
Wafugaji hao
walitoa msimamo huo katika mafunzo sheria ya ardhi ya mwaka 1999 yaliyoendeshwa
na Shirika la MPDO Lareto kwa ufadhili
wa The Fondation for civil Society na
kufanyika katika vijiji tisa vya wilaya hiyo.
Akizungumzia
mafunzo hayo diwani wa viti maalumu kutoka kata ya Selela Napir Engidong
alisema kuwa viongozi wa vijiji wameweza kufahamu umuhimu wa kutunza ardhi kwa
kupanda miti na kuacha ukataji miti hovyo.
“Upo umuhimu
mkubwa wa kushirikisha jamii katika kufanya maamuzi yanayohusu matumizi ya
ardhi, Kama wananchi watashirikishwa, migogoro mingi iliyopo vijiji itapungua”alisema Nengidong.
Naye Mkurugenzi
wa MPDO Baraka Laizer alisema kuwa waliendesha mafunzo hayo ili kuondoa
migogoro ambayo imekuwa ikisababaisha kukosekana kwa amani katika vijiji.
“Tumeshuhudia
watu wakipoteza maisha ,mali kuharibiwa kutokana na migogoro ya ardhi
,tumegundua kuwa njia pekee ya kuleta suluhu ni kwa viongozi na wadau
mbalimbali katika vijiji kuelimishwa kuhusu sheria ardhi ya vijiji”alisema
Baraka.
Kwa upande
wake mwezeshaji wa mafunzo hayo Amani Ole Sekino alisema kuwa viongozi wa
serikali za vijiji wameeelimshwa kuhusu sheria ya ardhi pamoja na utatuzi wa
migogoro kwa kuzingatia sheria.
Alisema kuwa
washiriki walifundishwa juu ya umilikaji wa ardhi ,umuhimu wa kuanisha mipaka
na kupata hati miliki ya ardhi ili kuilinda ardhi.
MWISHO……