Wednesday, December 19, 2012



Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe (kulia), akisisitiza wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akitoa taarifa ya mkutano wa Kamati Kuu ya chama hicho. Kushoto ni Katibu Mkuu wa chama hicho, Willibrod Slaa.
Kamati  Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), imebaini upungufu katika mchakato unaoendelea wa mabadiliko ya Katiba na kuiagiza Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutumia njia za kibunge kuhakikisha tume huru ya uchaguzi inapatikana na sheria zinazosimamia uchaguzi zinarekebishwa kabla ya Katiba Mpya haijaundwa mwaka 2014.

Njia hizo za kibunge, ambazo kambi hiyo inayoongozwa na Chadema bungeni inataka kuzitumia, ni pamoja na kuwasilisha hoja au miswada binafsi bungeni kupendekeza marekebisho ya katiba mpito ili kuhakikisha tume huru ya uchaguzi pamoja na marekebisho ya sheria hizo vinafanyika.

Tamko hilo lililotolewa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ni miongoni mwa maazimio 10, yaliyofikiwa na Kamati Kuu ya chama hicho, katika mkutano wake wa siku mbili uliohitimishwa Desemba 16, mwaka huu, jijini Dar es Salaam.

Mbowe, ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, alisoma maazimio hayo, alipozungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam jana.

“Kamati Kuu imepokea taarifa ya awali kuhusu mchakato wa katiba mpya na kubaini upungufu katika mchakato unaoendelea (wa mabadiliko ya katiba),” alisema Mbowe.

Alisema upungufu ambao Kamati Kuu imeubaini kuwapo kwenye mchakato wa mabadiliko ya katiba, unaweza kukwamisha upatikanaji wa Katiba Mpya na bora mwaka 2014 kama ilivyotangazwa na serikali na Tume ya Mabadiliko ya Katiba inayoongozwa na Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba.

Kutokana na hali hiyo, alisema Kamati Kuu imeazimia kwamba, kamati yake ndogo ikutane kwa haraka na kufanya tathmini zaidi na kutoa taarifa kwa umma kuhusu suala hilo.

“Aidha, kamati hiyo iwasilishe mapendekezo kwa tume ya mabadiliko ya katiba juu ya maoni ya Chadema ya kuzingatiwa katika katiba mpya na mapendekezo kwa serikali juu ya marekebisho ya sheria ya mabadiliko ya katiba awamu ya pili na ya tatu kwa pamoja ili nchi ipate katiba mpya na bora yenye mwafaka wa kitaifa,” alisema Mbowe.

Alisema wanahofu kwa mwendo ulivyo katika mchakato wa mabadiliko ya katiba, huenda Katiba Mpya isiwe tayari kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2014 na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Mbowe alisema hawana sababu ya kuiamini Tume ya Mabadiliko ya Katiba wala serikali kwa kuwa hakuna mtu anayejua kama majimbo ya uchaguzi yatakuwaje, viti maalum, Bunge nakadhalika.

Alisema hofu ambayo Jukwaa la Katiba iliyonayo kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba unavyokwenda ni ya msingi sana.

Mbowe alisema agizo la Kamati Kuu kwa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni limezingatia kuwa kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kura ya maoni ya Katiba Mpya itasimamiwa na tume ya sasa kwa mfumo wa kikatiba na kisheria usio huru.

Alitaka mchakato wa mabadiliko ya katiba usiwafunge Watanzania kufanya mambo mengine ya msingi kwa maslahi na usalama wa taifa, kama vile kuifanyia marekebisho Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na sheria zote zinazosimamia uchaguzi, ambazo zinaweza kuwa ni kikwazo cha kuwa uchaguzi huru na wa haki. 

“Uchaguzi wa hila na uchaguzi wa uchakachuaji hatutaukubali. Mwaka 2013 marekebisho ya sheria za uchaguzi yafanyike. Kwa sababu tumetumia mwaka 2011 na 2012 kujadili na kuipa muda serikali. Wasidhani tunacheza makida makida,” alisema Mbowe.

Alisema Sheria ya Uchaguzi, ambayo ni ya mwaka 1985, inapaswa kufanyiwa marekebisho kwa kuwa ina umri mrefu, ilitungwa kukiwa na mfumo wa chama kimoja na kwamba, tangu kipindi hicho, imefanyiwa marekebisho mara chache, hivyo imepitwa na wakati.

Mbowe alisema miongoni mwa mambo yanayoshawishi kutaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho ni pamoja na kutoruhusu Watanzania wanaoishi nje ya nchi kupiga kura katika uchaguzi kumchagua kiongozi wanayemtaka.

UCHAGUZI WA MADIWANI, MITAA

Mbowe, ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alisema Kamati Kuu pia imetaarifiwa juu ya kucheleweshwa kwa chaguzi za marudio za udiwani, mitaa, vijiji na vitongoji katika maeneo mbalimbali nchini.

Kutokana na hilo, alisema Kamati Kuu imeazimia kwamba, uongozi wa Chadema katika maeneo husika uunganishe umma kufanya shinikizo la kisiasa kwa mamlaka zinazohusika kutangaza nafasi hizo kuwa wazi na vyombo vinavyosimamia chaguzi katika ngazi hizo, ili haki za kikatiba na kisheria za wananchi kupata uwakilishi zipatikane kwa wakati.

DAFTARI LA WAPIGAKURA

Alisema pia Kamati Kuu ilizingatia hatua ya serikali na Nec kukwepa wajibu wa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapigakura (DKWK) tangu mwaka 2010.

Mbowe alisema hali hiyo inaathiri haki za wananchi kupiga kura na matokeo ya chaguzi za marudio zinazofanyika.
Hivyo, alisema Kamati Kuu imeazimia kwamba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ichukue hatua za kibunge kuhakikisha kwamba, DKWK) linaboreshwa mwaka 2013 ikizingatiwa kuwa daftari hilo hilo litatumika kwenye kura za maoni za Katiba Mpya.

HOJA ZA ZITTO, MDEE, LISSU

Alisema pia Kamati Kuu imetaarifiwa kuhusu hoja binafsi zilizowasilishwa na wabunge wa Chadema; Halima Mdee (Kawe) kuhusu ugawaji kiholela wa ardhi na Zitto Kabwe (Kigoma Kaskazini) kuhusu fedha zilizofichwa nje ya nchi na maazimio yaliyopitishwa an Bunge kuhusu hoja hizo.

Mbowe alisema pia imetaarifiwa kuhusu kusudio lililotolewa na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, kuhusu hoja ya uteuzi wenye kasoro wa baadhi ya majaji.

Kutokana na hali hiyo, alisema Kamati Kuu imeazimia kwamba, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni ifuatilie kwa karibu serikali kuhusu hoja hizo na kupendekeza hatua za ziada za Chadema kuwaunganisha wananchi iwapo hakutakuwa na uwajibikaji unaohitajika.

OPERESHENI M4C

Mkutano huo wa Kamati Kuu ulijadili ajenda mbalimbali, ikiwamo yatokanayo na mikutano yake miwili iliyopita, taarifa ya hali siasa, mapendekezo ya mwendelezo wa Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) na taarifa kuhusu mchakato wa mabadiliko ya katiba na kufanya maamuzi.

Alisema walizuia M4C ili kutoa fursa kwa Rais Jakaya Kikwete kujibu barua waliyomwandikia na mazungumzo waliyofanya juu ya hoja ya kuundwa Tume ya Kimahakama/Kijaji kuchunguza mauaji yaliyofanywa dhidi ya mwandishi wa habari aliyekuwa mwakilishi wa kituo cha televisheni ya Channel ten, marehemu Daudi Mwangosi.

Lakini alisema kutokana na kutopata majibu kwa zaidi ya miezi mitatu sasa, kuanzia Januari, mwakani, hawatasubiri tena majibu ya barua hiyo, badala yake watashinikiza wananchi kulaani mauaji hayo.

Alisema mwaka 2013 utakuwa ni mwaka wa nguvu ya umma na kwamba, M4C itatangazwa rasmi mwishoni mwa Januari, mwakani.

“Tunataka kwenda katika kila kituo ndani ya miezi 12 katika mwaka 2013,” alisema Mbowe na kuongeza: “Tumechoka kuibembeleza serikali,” alisema.

0 comments:

Post a Comment

Time Management

Translator

Popular Posts

Blog Archive

Fellow Bloggers

Popular Posts

Visitors Worldwide

Total Pageviews