Wednesday, December 5, 2012


 
Wakili  wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Vitalis Timon, ameiambia Mahakama ya Rufani kuwa waliopinga matokeo ya ubunge wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini (Chadema), Godbless Lema, hawakuwa na haki ya kufanya hivyo kisheria na kwamba matusi, kejeli na kashfa haviwezi kumvua nafasi hiyo.

Alidai kuwa matusi hayawezi kumvua ubunge Lema kwani wabunge wenyewe walitunga sheria namba nane ya mwaka 1995 ikiruhusu matusi baada ya kuona awali kuwa walikuwa wakibanwa na mahakama.

Wakili Timon alitoa madai hayo katika Mahakama ya Rufani mbele ya jopo la majaji watatu lililowajumuisha Jaji Nathalia Kimaro, Salum Massati na Benard Luanda, waliposikiliza rufaa iliyowasilishwa na Lema akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Arusha wa kumvua ubunge.

Lema alivuliwa ubunge Aprili 5 mwaka huu kufuatia kesi iliyofunguliwa na wanachama watatu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel.

“Wapiga kura hawawezi kupinga matokeo ya uchaguzi wakati yanayotokea katika kampeni hayawahusu, mpiga kura si sehemu ya kamati ya maadili na hana haki katika kampeni...katika ushahidi walalamikaji walidai kwamba walimshauri Batilda (aliyekuwa mgombea wa CCM) kwa muda mrefu afike mahakamani, alikataa ndipo wakaamua kwenda wao mahakamani,” alidai na kuongeza kuwa:

“Julai 31, 1995 Bunge lilipitisha sheria namba nane wakisema kwamba matusi si sababu ya kutengua matokeo, wenyewe Wabunge waliruhusu watukanane katika sheria waliyotunga, wanapenda kutukanana, wabunge walijipendelea wakati wakitunga sheria hiyo baada ya kuona mahakama inawabana katika eneo hilo, waacheni watukanane waliyataka wenyewe,” alidai wakili huyo mwandamizi wa serikali.

Timon alidai kuwa wanaohusika wakati wa kampeni ni wagombea, vyama vya siasa, mawakala wa wagombea na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) na kwamba wapiga kura wanahusika kulalamikia hatua za usajili wa wapiga kura na wakati wa kupiga kura.

 “Waheshimiwa majaji, waliokuwa na maslahi binafsi katika kesi hii ni waliopoteza jimbo. Baada ya uchaguzi CCM walikaa kikao na kuazimia kulirudisha jimbo kwa kufungua kesi, walikuwa na nia mbaya walipofungua shauri hili,” aliendelea kuieleza mahakama.

“Sioni kwa nini Jaji wa Arusha aseme Lema alikuwa na maslahi binafsi katika ushahidi wake kwa kuleta wanachama wa Chadema kutoa ushahidi, angewaleta watu gani zaidi ya hao waliokuwapo wakati wa kampeni?” alihoji.

 “CCM walileta mashahidi wa CCM, lakini hawakuambiwa kwamba walikuwa na maslahi binafsi, naunga mkono rufaa na naomba uamuzi wa kumvua Lema ubunge utenguliwe,” aliiambia mahakama.

Wakili wa Lema, Method Kimomogolo, akizungumzia hoja 18 za kukata rufaa hiyo, alidai kwamba Jaji aliyetoa hukumu ya kumvua ubunge Lema, Gabriel Rwakibarila, alikosea kisheria kuvutiwa na njia walizotumia shahidi wa 11 na 14 badala ya kuzingatia uzito wa ushahidi waliotoa.

 “Alivutiwa na shahidi wa 11 Amina Ally ambaye anaishi kwa kuuza mitumba na shahidi wa 14 ambaye alitumikia jeshi nje ya nchi na akastaafu kwa kuogopa kupelekwa tena nje ya nchi,” alidai Kimomogolo.

“Jaji alikosea kuegemea katika ushahidi usioaminika na ushahidi wa mdomo bila kutafuta ushahidi mwingine wa kuunga mkono hivyo kuifanya hukumu kutokidhi vigezo vya kuitwa hukumu,” alidai Kimomogolo.

Kimomogolo alidai kuwa Jaji Rwakibarila wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga katika hukumu yake hakutumia mifano ya kesi mbalimbali zilizoamuliwa na Mahakama ya Rufaa, japo alipelekewa ili azirejee na mawakili wa pande zote mbili.

Kimomogolo aliendelea kulieleza jopo hilo la majaji kuwa Jaji Rwakibarila hakuchanganua wala kupima ushahidi licha ya kuwasilishiwa viini vikuu vilivyokuwa vinabishaniwa.

“Mrufani hakuwahi kukamatwa na Polisi wakati wa kampeni kwa kutukana na jaji hakusema makosa gani ya jinai yalitendwa na mrufani katika kampeni zake,” alidai.

Alidai kuwa uamuzi uliomvua ubunge Lema ukikubaliwa na kuruhusu kila mtu apinge matokeo ya uchaguzi kwa kufungua kesi, hali itakuwa mbaya na kuongeza kuwa mtu afike mahakamani kwa malalamiko yanayomhusu.

“Jukumu la kutetea maslahi ya Taifa ni la Mwanasheria Mkuu wa Serikali, si wanachama wa CCM waliopinga ubunge, kama wanaona AG hafanyi kazi vizuri, wananchi wamwajibishe,” alidai.

Wakili Kimomogolo alirejea kesi mbalimbali zinazofanana na kesi ya Lema ikiwamo ya Joseph Warioba dhidi ya Stephen Wassira, Basil Mramba dhidi ya Leonce Ngalai, William Bakari dhidi ya Mgonja na kesi ya Walid Kabourou  iliyoamuliwa miaka 16 iliyopita na watu waliwasilisha hadi `tape' mahakamani.

“Kwa nini katika kesi ya Lema wajibu rufani hawakuwasilisha hata ushahidi wa `tape' kuonyesha matusi aliyotukana?” alihoji Kimomogolo.

Wakili wa wajibu rufani, Alute Mughway, alidai mashahidi wao walieleza kila kitu mahakamani na jaji alikuwa anajua nani mwenye jukumu la kuthibitisha kesi.

Alidai kuwa ushahidi uliotolewa haukupaswa kuungwa mkono na ushahidi wowote na kwamba siasa za uchaguzi zinatakiwa kuwa safi kwani hata katika kanuni za uchaguzi wanaonywa kuhusu matusi, kejeli na kudhalilishana.

“Siasa za matusi ni siasa za maji taka zilikatazwa, kanuni zilizokataza zilisainiwa na vyama vyote, watu wanachaguliwa kwa hoja si kungurumisha matusi na kuwadhalilisha wagombea wengine,” alidai Mughway.

Alidai kuwa hukumu ilikidhi viwango vyote na kuomba rufaa itupiliwe mbali kwa sababu zilizotolewa na mrufani hazitoshelezi kutengua uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.

“Waheshiwa, tunaomba uamuzi wa Mahakama ya Arusha ubaki kama ulivyokuwa na warufani waamuriwe kulipa gharama za kesi,” alidai. Kesi iliahirishwa hadi tarehe ya hukumu itakapopangwa.

 Akizungumza katika viunga vya mahakama hiyo baada ya kuahirishwa kesi hiyo, Lema aliwasihi wanachama wake kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu wakati wanasubiri hukumu.

“Hiki ni kipindi kigumu wakati tunasubiri hukumu kutolewa kuliko tulipokuwa tunasubiri usikilizwaji wa rufaa hii, nawasihi muwe na utulivu kwani kila mmoja amesikia mahakamani mawakili walivyotoa hoja zao,” alidai Lema.

Aliwataka kuwa watulivu waiachie mahakama ifanye kazi yake kwa mujibu wa sheria na kwamba haki itatendeka.

Mapema saa 2:00 asubuhi, viunga vya mahakama hiyo vilifurika wafuasi wa Chadema wakiongozwa na Lema waliofika kusikiliza kesi hiyo pamoja na wananchi mbalimbali.

Ukumbi namba moja wa mahakama hiyo ulifunguliwa saa 2:30 asubuhi na saa 3:00 asubuhi  jopo hilo liliketi chini na kuanza kusikiliza hoja za mawakili wa pande zote mbili.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi jopo litakapopanga tarehe ya hukumu kama Lema atarudishiwa ubunge wake ama la.

0 comments:

Post a Comment

Time Management

Translator

Popular Posts

Blog Archive

Fellow Bloggers

Popular Posts

Visitors Worldwide

Total Pageviews