Sunday, November 11, 2012
Spika wa Bunge, Anne Makinda,  amesema shughuli za Bunge ni mzigo mzito.
Hata hivyo, amesema uwajibikaji wa watumishi wa muhimili huo wamemwezesha kufanya kazi zake vizuri.

Makinda aliyasema hayo juzi usiku wakati wa hafla ya kuwaaga wafanyakazi waliostaafu na kuwakaribisha waajiriwa wapya wa Bunge.

Makinda hakueleza kwa undani namna shughuli za Bunge zinavyokuwa mzigo, lakini mara kadhaa, uongozi wake umekuwa ukikosolewa ndani na nje ya chombo hicho cha uwakilishi wa wananchi.

Aidha, aliwataka watumishi wapya, kuwaheshimu wabunge na kujitahidi kutowakosea wakati wa utendaji wao wa kazi ili kuepuka malalamiko.
“Hata kama wamefanya vibaya wao, omba samahani maana ukimjibu vibaya itakuwa nongwa tena nongwa kweli kweli,”alisema.

Makinda aliwataka watumishi wa Bunge waliostaafu, kujishughulisha na miradi mbalimbali ya maendeleo itakayosaidia kuwaongezea kipato badala ya kukaa bila kazi.
“Mzee wa miaka 60 si mzee anayeweza kufanya kazi nyingine kama kuuza mitumba, nyanya…msifunge akili zenu kwa sababu kuishi na wenzenu waliowazunguka vizuri kutafanya msizeeke,”alisema.
Makinda aliwasihi wastaafu hao kuweka fedha zao za mafao benki ili wapate muda wa kufikiria watazitumia vipi.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Utawala wa Bunge, Kitolipa Kipa, alisema jumla ya watumishi 19 wameajiriwa na 13 wamestaafu.
“Wenzetu tunaowaaga leo (juzi) walifanya kazi kwa uaminifu, uadilifu na baada ya kupita katika misukosuko, na dhoruba,”alisema.
Aidha, aliwataka wafanyakazi wapya kufanya kazi kwa bidii na kujituma ili waweze kulijenga Taifa.
Katika hafla hiyo pamoja na zawadi nyingine kila mtumishi alizawadia shilingi milioni 8.1.   
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 comments:

Post a Comment

Time Management

Translator

Popular Posts

Blog Archive

Follow by Email

Fellow Bloggers

Google+ Followers

Popular Posts

Visitors Worldwide

Total Pageviews