Monday, November 12, 2012

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Elias Lali


SILAHA, zaidi ya 80 za kivita zikiwemo aina ya  SMG na AK 47 zimesalimishwa kwa polisi  na wananchi wa vijiji mbalimbali katika tarafa ya Sale na Loliondo  Wilayani Ngorongoro Mkoani Arusha.

Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Elias Wawa Lali alisema kuwa silaha hizo zimesalimishwa  polisi kufuatia kampeni ya kuwataka watu wanaomiliki silaha kinyume na sheria kuzisalimisha kabla ya kukamatwa na kufikishwa mahakamani.

Alieleza kuwa silaha hizo zimekuwa zikitumika katika ugomvi kati ya wamasai na wasonjo hali ambayo ilikuwa inatishia hali ya usalama katika eneo la Loliondo.
“Watu wengi wakiwemo wanawake na watoto wamekuwa wahanga wakubwa wa migogoro hii ,serikali sasa imeazimia kumaliza migogoro hii kwa kutumia njia zote zikiwemo za usuluhishi na kisheria”alisema.

Alisema kuwa katika operesheni hiyo watu saba wanashikiliwa na polisi kwa thuma za kukutwa na ngombe ishirini na tisa mali ya wafugaji wa kimasai ambao waliporwa mwezi September mwaka huu katika kijiji cha Naan.

“ Majina yao tutayatoa baadaye ila ngombe walioporwa katika tukio hilo tumezikamata ndani ya msitu katika eneo la wasonjo  na  tayari wamiliki wake wamezitambua  na watuhumiwa tayari wapo mikononi mwa polisi”alisema Lali.

Lali aliongeza kuwa serikali Wilayani humo inaendelea kutoa elimu na ushawishi kupitia taasisi zake ili kuwafanya wananchi kuelewa kuwa kumiliki silaha bila kibali cha kisheria ni kosa la jinai.  

“Tunafanya kila tunaloweza kutokomeza  tabia ya watu kujimilikisha silaha ,nchi yetu inaongozwa kwa utawala wa sheria  haiwezekani wananchi wa kawaida kumiliki silaha za kivita”alisema Lali.

Aidha Mkuu huyo wa Wilaya aliongeza kuwa serikali inatarajiwa kutuma msuluhishi wa migogoro ya ardhi ambayo imekuwa ndio chanzo cha vita vya Wamasai na Wasonjo vita ambavyo vimegharimu maisha ya watu wengi.

“Wakati wowote wizara itamleta msuluhishi wa migogoro ya mipaka katika eneo lote la Lolindo ,tunaamini suala la mipaka likipatiwa ufumbuzi migogoro na vita vitakwisha katika eneo hili”alisema Lali.

0 comments:

Post a Comment

Time Management

Translator

Popular Posts

Blog Archive

Follow by Email

Fellow Bloggers

Google+ Followers

Popular Posts

Visitors Worldwide

Total Pageviews